Ubakaji na unyanyasaji wa kimapenzi au kijinsia ni makosa makubwa ya jinai hapa nchini Finland

Baadhi ya jamii zina utamaduni uliojengwa na wenye kukubaliana na dhana ya kwamba mwanamke aneyetembea nje akiwa pekee yake, au ikionekana wazi kuwa amelewa japo kidogo, basi huyo ni mwanamke mbaya na mwenye tabia mbovu isiyofaa. Kwako wewe unayetokea nchi ambako kuna mazoea, tabia, na fikira kama hizi, ni vema ujue ya kwamba, katika hili, hapa Finland mambo yanaangaliwa tofauti na huko ulikotokea.

Nchini Finland usawa na fikira kati ya mwanaume na mwanamke katika mazingira na mahusiano kama haya yanachukua mtazamo na maana tofauti. Ni kwamba mwanamke anaweza kuwepo kwenye disko au baa na akaonekana kabisa amelewa kiasi fulani, hata kama mwanamke siyo malaya. Ndiyo maana, kwa kuona hivyo wala usidhani kwamba wewe au mwanaume mwingine anayo haki ya kumlazimisha kufanya naye mapenzi, hata kwa kutumia nguvu. Nchini Finland hali ya mtu kuonekana amelewa pombe haina maana ya kuwa yeye amejawa na wazo la kutaka kufanya mapenzi, bali suala zima linahusiana na mwenendo na hali ya watu wa nchi hii kuhusiana na matumizi ya pombe. Msimamo, mtazamo, na mwenendo huu umejengwa juu ya mazingira ya utamaduni unaowafanya watu wa nchi hii kutokuwa na msimamo mkali dhidi unywaji wa pombe. Ndiposa utakuta vijana wanakunywa pombe vikali sana na ndiyo maaana, kwa bahati mbaya, watu wengi wamekuwa watumwa wa ulevi huu wa pombe.  

Hii yote huamsha makwazo na kuwaudhi wengi, sanasana wale wenye asili ya utamaduni wa kiislamu. Kusema kweli watu wa Finland wanakunywa kupita kiasi na hii husababisha matatizo mengi na makubwa sana.

Hata hivyo, ni vizuri kujua tofauti katika mambo haya. Kumlazimisha mwanamke kufanya mapenzi naye bila matakwa yake, kumtumia vibaya akiwa amelewa pombe, au hata akiwa ametumia madawa ya kulevya, yote haya ni makosa makubwa sana ya jinai nchini Finkand na hivyo basi, ni kwamba kila anayekosa na kuvunja sheria hii yeye mwenyewe ndiye anayelazimika kuwajibika na kuchukuliwa hatua kali kisheria. Pengine katika nchi unayotoka wewe inawezekana mwanaume kusingizia kwamba kosa ni lake yeye mwanamke anapotokewa na mabaya kama haya, na tena kwamba amestahili kutumiwa vibaya (yaani kulazimishwa kufanya mapenzi kinyume na matakwa yake) eti kwa sababu yeye ni mwanamke mwovu asiyekuwa na heshima, na tena kwa kisingizio cha kuwa yeye mwanamke ameyataka mwenyewe.

Pia kwenye dini yako yawezekana wanawake wanalinganishwa, pia kuhusishwa na ubaya (uovu) na ya kwamba wanaweza kutumiwa ovyo na holela tu bila kujali haki yao kisheria. Kwenye dini yako hali ya kufanya mapenzi au tendo la ndoa, pamoja na mtu kuumbwa mwanamke vyote huonekana kana kwamba ni uchafu, na ya kwamba wanaume wenyewe ndio wasafi, hivyo wao hujaribiwa tu na uovu wa wanawake ndio maana wanawatongoza wanawake. Kwenye nchi uliyotoka wewe, nafasi ya mwanaume yawezekana ikawa ya juu zaidi mbele ya sheria pale anapokuwa ameshtakiwa na mwanamke kwa kosa la kumbaka yeye mwanamke. Nchini Finland, hata hivyo, mambo ni kinyume chake kisheria. Hapa matendo ya mtu hupimwa kisheria kulingana na sheria yenyewe, tena mbele ya sheria ya nchi hii. Dini au utamaduni wa kale haviwezi kutumika kumwokoa mtu asipewe adhabu inayotokana kitendo chake kibaya cha kuvunja sheria. Nchini Finland hata mke wako mwenyewe wa ndoa uliyemuoa ukimlazimisha kufanya mapenzi nawe kwa nguvu, hii itahesabiwa ni ubakaji, na ni kosa la jinai linalostahili adhabu. 

Sasa basi, vijana ni lazima wajifunze mambo mbalimbali muhimu ya msingi kuhusu mahusiano ya kimapenzi, ili kwamba wasije wakajawa na habari na mawazo ya kupotosha yanayoweza kuwafanya wavunje sheria mara watakapoanza kupata hamu na mvuto kujihusisha na masuala ya kimapenzi. Cha muhimu wangejifunza zaidi kuheshimiana na watu wengine, kuthamini usawa kwa wote, na kujilinda dhidi ya kutumiwa vibaya na kudhalilishwa kimapenzi. Kufanya mapenzi, kama tendo, siyo kitu kibaya, bali ni sehemu ya ubinadamu. Kwa hali hii haifai kufikiri eti mwanaume ndiye msafi zaidi kuliko mwanamke. Wala hakuna utamaduni, dini, au watu wa nchi fulani ambao ndio wasafi kuliko wenzao wengine. Hakuna mwenye haki ya kumlazimisha kwa nguvu au kumshawishi mtu mwingine afanye naye mapenzi bila idhini na matakwa ya huyo mwingine. Ifahamike pia kwamba, tendo la kufanya mapenzi, yaani tendo la ndoa, kati ya mtu mzima na mtoto aliye chini ya umri wa miaka 16 ni kosa la jinai nchini Finland, na huweza kusababisha mtu apate adhabu ya kifungo cha jela. Pia kumtumia vibaya mtoto mdogo kwa nia ya kujifurahisha na kuridhisha kimapenzi ni kosa kubwa sana la jinai hapa Finland, na anayepatikana na hatia kama hiyo aweza kupelekwa jela na kufungwa. Kama umejifunza kufikiria mambo kwa msimamo mwingine mkali tofauti, inawezekana chanzo chake, kwa mfano, kikawa ni ukweli kwamba wale waliokukuza na kukufundisha hawakujua mambo mengine yanayoendelea sehemu zingine zilizo mbali na mazingira uliyokulia wewe. Mawazo yasiyostahili na yasiyofaa yakitokea mahali pasipofaa yaweza hata hivyo kusababisha mtu kujihusisha na vitendo vibaya vya ajabu ajabu na hata vikamletea matokeo na madhara makubwa mabaya.

Majira yaliyopita (ya baridi) kulitokea vitendo vingi vya ubakaji mjini Oulu, ambapo ilibainika kuwa wakosaji walikuwa ni wanaume wenye asili ya nchi za kigeni (yaani wanaume wageni au wahamiaji) ambapo waliofanyiwa uovu walikuwa wanawake raia wa Finland. Makosa yenyewe ya jinai yalikuwa ya kikatili mno, kwa mfano katika tukio moja wabakaji walitumia hadi mkasi, wakati ambapo matukio mengine mawili yalihusisha kundi zima kufanya ubakaji. Kwa kweli makosa yanayofanana na haya huibua chuki ndani ya wazawa wa Finland na huwafanya wawe na kasumba mbaya dhidi ya watu watokao nchi zingine kuja kuishi au kukaa hapa. Chuki na kasumba kama hii inapokua na kuenea zaidi katika jamii, matokeo yake ni matatizo makubwa sana kwa watu wote wanaohamia nchi hii kutoka nchi za nje; kwa mfano tu inakuwa ngumu kupata kazi, hawawezi kuchukuliwa sawa na wengine, na hata hali ya usalama kwa ujumla itazidi kuwa mbaya pale ambapo wazawa wa Finland wenye kutumia zaidi ubabe na nguvu watataka kupambana na kukabiliana na vitendo viovu vya wahamiaji wasiojiheshimu. Kwa ujumla, ubaguzi wa rangi ukikua na kukomaa, na hata kuenea zaidi, hamu itaondoka kabisa ya kuwakubali wahahamiaji wageni kutoka nchi zingine kuja nchi hii, kuishi jirani na wazalendo itakuwa ngumu, au hata kupatiwa kazi itakuwa shida.

Na wewe ukiwa kama mzazi una jukumu kubwa sana na wajibu kuhakikisha unawaelekeza vijana wako, ili wasije wakamlazimisha mtu yeyote kufanya naye mapenzi bila matakwa yake huyo mtu. Watu ni lazima waheshimiane, hata kama wako tofauti kiasi gani. Mwenendo mzima, tabia, na hali ya watu wa Finland kuhusu matumizi ya pombe, pamoja na tabia ya wanawake inaweza, labda, ikakusababisha uelewe mambo tofauti na yale uliyazoea kuyaona huko ulikotoka.

Imeandaliwa na Ofisi ya Huduma kwa Wahamiaj

Käännös: Keski-Suomen tulkkikeskus